Jumanne, 27 Mei 2014

David Luiz ni Shidaa

BEKI, Mbrazili David Luiz, anasema kwamba anaondoka Chelsea akiwa na masikitiko makubwa. Staa huyo amefuzu vipimo vya afya na kufikia makubaliano binafsi na klabu ya Paris Saint-Germain kwenye uhamisho wake uliowagharimu mabingwa hao wa Ufaransa Pauni 50 milioni.
Uhamisho huo unamfanya Luiz kuwa beki ghali zaidi duniani na kuvunja rekodi za mabeki wengine kadhaa waliowahi kuhamishwa kwa pesa nyingi kwenye mchezo huo wa soka.
Ilichokifanya PSG ni kama Real Madrid ilipovunja rekodi ya Cristiano Ronaldo ya Pauni 80 milioni kwa kumnunua Gareth Bale kwa Pauni 86 milioni baada ya mabeki waliokuwa wakishikilia rekodi ya kuwa ghali duniani ni Marquinhos na Thiago Silva.
Luiz apandiwa ndege
Baada ya Chelsea kukubali kufanya biashara na PSG, mabosi wa klabu hiyo tajiri ya Ufaransa iliwapandisha ndege wawakilishi wake nchini Brazil kwenda kumpima afya Luiz ili kukabilisha dili hilo.
Tukio hilo hilo lilifanyika Ijumaa iliyopita wakati Luiz alipokuwa kwenye kambi ya timu ya taifa ya Brazil inayojiandaa na fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika kwenye ardhi ya nchi hiyo kuanzia mwezi ujao.
Baada ya klabu ya Chelsea kuthibitisha kupitia kwenye tovuti yake kwamba imemuuza Luiz, staa huyo Mbrazil alifichua kuumia kwa uhamisho huo kwa sababu aliishi Stamford Bridge kwa karibu miaka minne na amezoea sana mahali hapo.
“Nawashukuru Chelsea kwa kipindi chote za miaka mitatu na nusu niliyokaa mahali hapo. Nimepata ushirikiano mkubwa sana.
Nawashukuru wachezaji wenzangu, mabosi na mashabiki. Naondoka kwa huzuni kubwa, lakini pia nafurahia changamoto hii kwa kujiunga na klabu kubwa na inayojaribu kujipanga zaidi,” alisema.
PSG inaamini kwamba imemnasa moja ya mabeki wa maana sana duniani na kwamba itaendelea kutumia pesa kusajili wakali wengine baada ya fainali za Kombe la Dunia.
Mabeki wengine ghali
Uhamisho wa Luiz unavunja rekodi za uhamisho ghali wa mabeki wengi sana na kwenye orodha hiyo wamo, Thiago Silva aliyehama AC Milan kwenda PSG kwa Pauni 35.3 milioni, Marquinhos (Roma kwenda PSG) kwa pauni 30.1 milioni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni